Maadhimisho ya siku ya nyuki duniani yalifanyika kitaifa mkoani Singida, katika viwanja vya Bombadia. Maadhimisho hayo yaliambatana na maonesho yaliyoanza tarehe 18/5/2023 na kufikia kilele chake tarehe 21/5/2023. Wadau mbalimbali walihudhuria maadhimisho hayo, ikiwemo wawakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Kampasi ya Mizengo Pinda. Kampasi hiyo ni mdau muhimu sana kwa kuwa inatoa Shahada ya Usimamizi wa Rasilimali za Nyuki. Maadhimisho ya mwaka huu yalikua na kaulimbiu isemayo, “Tuwalinde Nyuki kwa Ustawi wa Mazingira na Usalama wa Chakula.”
Wawakilishi kutoka Kampasi ya Mizengo Pinda walipata fursa ya kuwasilisha mada mbalimbali kwa wadau wa nyuki waliojitokeza kwenye maonesho hayo. Bw. Joseph Ruboha alizungumzia “Athari za Viuatilifu kwa Wadudu Wachavushaji Hasa Nyuki.” Alisema kwamba kumekuwa na ongezeko la matumizi ya viuatilifu, hususani kwenye shughuli za kilimo. Hata hivyo, viuatilifu hivi vina athari kwa nyuki na wadudu wengine wachavushaji. Athari zinazoweza kuwapata nyuki ni pamoja na kufa kwa nyuki, kuanguka kwa koloni, kubadilika kwa tabia za nyuki, na kupungua kwa mimea ambayo nyuki huitumia kutengeneza rasilimali zao. Madhara haya hayaishii kwa nyuki tu, kwani kukosekana kwa nyuki kunahatarisha usalama wa chakula na mazingira.
Njia mbadala endelevu zinashauriwa ili kupunguza athari za hivi viuatilifu kwa nyuki na wachavushaji wengine. Njia hizi ni pamoja na kutumia njia za asili kama vile kutumia mbegu zilizoboreshwa ili kuhimili wadudu wasumbufu, kutumia dawa za asili, na kutumia mitego maalum kwa wadudu wasumbufu. Pia, kufuata miongozo ya kusimamia makoloni ya nyuki wa asali iliyowekwa na wizara.
Kwa upande mwingine, Bi. Dorothea Kipangula alizungumzia faida za Nyuki katika usalama wa chakula. Kwenye mada hiyo alielezea jinsi gani nyuki wana umuhimu katika usalama wa chakula na wanavyochangia hasa katika uchavushaji wa mazao muhimu hapa Nchini. Bi Dorothea alimalizia kwa kusema kuwa nyuki ni muhimu sana katika usalama wa chakula, uchumi, na mfumo wa ikolojia. Ni muhimu kulinda na kuhifadhi nyuki na makazi yao ili kuhakikisha kuwa tunaweza kuendelea kunufaika na huduma muhimu ambazo wanatoa.