Madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Urambo wamefanya ziara fupi katika Kampasi ya Mizengo Pinda ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo. Katika ziara hiyo, madiwani hao waliongozana na mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo pamoja na mwenyeji wao mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mh. Silas Ilumba na mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Bi. Catherine Mashalla.
Pamoja na mambo mengine, madiwani hao walikua na kiu kubwa ya kufahamu kuhusu ufugaji wa kisasa na wa kitaalamu wa nyuki pamoja na shughuli na kozi mbalimbali zitolewazo na Kampasi ya Mizengo Pinda.
Akifungua kikao kifupi pamoja na madiwani hao, Rasi wa Kampasi ya Mizengo Pinda, Prof. Josiah Katani, alitoa maelezo mafupi kuhusu kozi tatu zitolewazo katika Kampasi ya Mizengo Pinda na fursa nyingi zinazojitokeza kutokana na uwepo wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Kilimo katika Halmashauri ya Mpimbwe.
Kwa upande mwingine, Bw. Evaristus Magani, Mhadhiri Msaidizi, alizungumzia faida za ufugaji wa kisasa wa nyuki, maeneo mbalimbali ambayo mtu anaweza kufugia nyuki hata kama hana eneo la kibinafsi na mazao mbalimbali ya nyuki kama vile asali, nta, chavua na sumu ya nyuki. Pia alieleza kwamba mazao ya nyuki yanaweza kuchakatwa na kuongezewa thamani ili kuzalisha bidhaa nyingine nyingi ikiwemo sabuni, dawa za kung’arishia viatu, vipodozi n.k.
Bw. Magani alimalizia kwa kuzungumzia jinsi ufugaji wa nyuki ulivyo na manufaa makubwa katika kutunza mazingira na kwenye kuongeza uzalishaji wa mazao kupitia huduma ya uchavushaji.
Naftari Josephat, mwanafunzi wa Shahada ya Usimamizi wa Rasilimali za Nyuki, alitoa maelezo mafupi kuhusu sumu ya nyuki. Alifafanua jinsi sumu hiyo inavyovunwa, manufaa yake, soko lake. Hili ni zao la nyuki ambalo linaweza kuvunwa muda wowote ambao mfugaji anataka kuvuna.
Naftari Josephat, Mwanafunzi wa Shahada ya Usimamizi wa Rasilimali za Nyuki, Akieleza Jinsi ya Kukusanya Sumu ya Nyuki, Umuhimu Wake na Soko Lake