Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda afanya ziara katika Kampasi ya Mizengo Pinda

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Prof. Raphael Chibunda, amefanya ziara ya kutembelea Kampasi ya Mizengo Pinda. Lengo kuu la ziara hiyo likiwa ni kusikiliza kero, kushughulikia changamoto za watumishi, na kutathimini maeneo ambayo yatajengwa majengo mapya matatu kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET). Majengo hayo ni pamoja na Jengo la Taaluma, Bwalo, na Daharia.

Prof. Chibunda ametoa wito kwa watumishi wa Kampasi ya Mizengo Pinda kushirikiana kwa karibu katika kutekeleza majukumu yao na kuendeleza utamaduni wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kuwa kielelezo bora kwa jamii inayowazunguka.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda akiongea na Watumishi wa  Kampasi ya Mizengo Pinda

Katika ziara hiyo, Profesa Chibunda aliambatana na Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), Dkt. Winfried Mbungu, ambaye naye alipata nafasi ya kutoa taarifa ya maendeleo ya mradi. Dkt. Mbungu alithibitisha kwamba katika Kampasi ya Mizengo Pinda yatajengwa majengo matatu kama sehemu ya mradi huo, yaani Jengo la Taaluma, Bwalo, na Daharia. Aliongeza kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati uliopangwa.

Dkt. Mbungu alielezea pia mradi wa HEET si tu unashughulika na kujenga majengo mapya, bali unadhamini mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ambapo ametoa wito kwa watumishi wa Kampasi ya Mizengo Pinda kutumia fursa hii kujipatia elimu zaidi. Pia, alibainisha mafanikio ya baadhi ya watumishi ambao wameshafaidika na udhamini wa kielimu kupitia mradi huo.

Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) Dkt. Winfried Mbungu akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa HEET

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala, Mipango, na Fedha, Prof. Amandus Muhairwa aliyekuwa ameambatana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Prof. Raphael Chibunda katika ziara hiyo, alipongeza utaratibu wa utendaji kazini wa watumishi wa Kampasi ya Mizengo Pinda. Hata hivyo, alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa watumishi hao kutumia vyema ofisi zao wanapokutana na changamoto au wanapohitaji ufafanuzi wa taarifa yoyote inayohusiana na masuala ya kazi. Prof. Muhairwa aliwahimiza kuacha tabia ya kuziogopa ofisi hizo na badala yake kuziona kama sehemu muhimu ya kutatua matatizo yao.

Aidha, katika kusisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala, Mipango, na Fedha, Prof. Amandus Muhairwa, alizungumzia suala la wafanyakazi kupata stahiki zao kwa wakati. Prof. Muhairwa alifafanua kuwa wafanyakazi wote wenye madai yao wataweza kuyapata kikamilifu, na kuwahimiza watumishi hao kufika katika ofisi za usimamizi wa rasilimali watu kwa maelezo kamili na kuhakikisha mchakato wa malipo unakuwa wa haraka na wenye ufanisi.

Pamoja na hayo, Prof. Muhairwa alisisitiza umuhimu wa watumishi wa Kampasi ya Mizengo Pinda kuwa na utaratibu wa kuwahi ofisini. Hii ni kwa lengo la kufanya kazi kwa weledi na kutimiza vyema majukumu yao kama watumishi wa umma. Alisisitiza kuwa kuwepo ofisini kwa wakati ni sehemu muhimu ya kujenga utamaduni wa uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala, Mipango, na Fedha, Prof. Amandus Muhairwa akiongea na Watumishi wa  Kampasi ya Mizengo Pinda

Katika hatua nyingine, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, anayeshughulikia Taaluma na Utafiti, Prof. Maulid Mwatawala, ametoa wito kwa wanataaluma kuzingatia misingi ya ufundishaji. Alisisitiza umuhimu wa kufuata utamaduni, utaratibu, na muongozo wa chuo katika mchakato wa kufundisha, akieleza kuwa hii ni njia muhimu ya kuzalisha wataalamu wenye tija kwa maendeleo ya taifa letu.

Prof. Mwatawala pia alieleza kwamba chuo kinaendelea na zoezi la kuboresha mtaala wa masomo. Katika muktadha huo, alitangaza kuwa Kampasi ya Mizengo Pinda imedhamiria kuongeza idadi ya programu zitakazokuwa zinatolewa katika Kampasi ya Mizengo Pinda. Hii inalenga si tu kuongeza idadi ya wanafunzi katika kampasi hii, bali pia kuchangia katika kukuza maendeleo ya kiuchumi katika jamii inayozunguka chuo na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Profesa Mwatawala alihamasisha ushirikiano wa karibu kati ya wanataaluma na wanafunzi kwa lengo la kufikia malengo ya ubora wa kitaaluma. Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu inayokidhi viwango vya kimataifa na kuzingatia mahitaji ya soko la ajira. Alimalizia kwa kutoa wito kwa wanataaluma kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko chanya na kujenga msingi imara wa elimu ya juu nchini.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, anayeshughulikia Taaluma na Utafiti Prof. Maulid Mwatawala akiongea na Watumishi wa  Kampasi ya Mizengo Pinda

Baadhi ya watumishi wa Kampasi ya Mizengo Pinda wakichangia mada na kuomba ufafanuzi wa baadhi ya mambo mbele ya Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)

Baada ya kumalizika kwa mkutano na watumishi wa Kampasi ya Mizengo Pinda, Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ilipata fursa ya kutembelea eneo ambapo majengo matatu muhimu yatajengwa. Majengo hayo ni Jengo la Taaluma, Bwalo, na Daharia.

Wakiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Raphael Chibunda, Menejimenti ilifanya ukaguzi wa kina wa maeneo hayo. Profesa Chibunda aliwaelekeza wajenzi na wahusika wengine kuhusu mahitaji na viwango vinavyohitajika kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa ubora na kwa wakati.

Aidha, wakati wa ziara hiyo, Profesa Chibunda aliwapa watumishi na wajenzi moyo wa kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa mafanikio. Alisisitiza umuhimu wa majengo hayo katika kuboresha miundombinu ya kielimu na kuongeza uwezo wa chuo kutoa huduma bora kwa wanafunzi.

Baadhi ya picha za matukio wakati wa ukaguzi wa maeneo ambapo majengo matatu muhimu yatajengwa kupitia mradi wa HEET

 

Related Posts

Former Prime Minister Mizengo Pinda Visits Mizengo Pinda Campus to Observe Development Activities

The Mizengo Pinda Campus of Sokoine University of Agriculture (SUA) in Katavi recently hosted an esteemed visitor, Hon. Mizengo Pinda,...

Learning Through Practice: SUA Students Visit Weather Station

At the Sokoine University of Agriculture (SUA) Mizengo Pinda Campus, the focus on experiential learning continues to set students apart...

SUA Kampasi ya Mizengo Pinda Yasheherekea Miaka 63 ya Uhuru Katika Mdahalo Ulioandaliwa na Halmashauri ya Mpimbwe

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda, Ndg. Joseph Oswald Ruboha, akitoa mada ya...