Prof. Chibunda amewataka watumishi wa Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo Kampasi ya Mizengo Pinda kufanyakazi kwa ushirikiano ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika kampasi hiyo. Aliyasema hayo alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika Kampasi ya Mizengo Pinda Novemba 7 – 8, 2022.
Katika ziara hiyo, Prof. Chibunda alipokea ripoti ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kampasi hiyo na kupata fursa ya kutembelea miradi hiyo.
Pia, Prof. Chibunda aliongeza kusema kwamba kupitia serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuboresha sekta ya elimu ya juu nchini ikiwemo Kampasi ya Mizengo Pinda. Kiasi cha pesa takribani bilioni ishirini zimetengwa kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza Kampasi ya Mizengo Pinda. Pesa hizo zinatarajiwa kutumika kujenga majengo matatu ambayo ni jengo la Taaluma linalokadiriwa kuchukua wanafunzi zaidi ya elfu mbili (2000) kwa wakati mmoja, maabara za kufundishia pamoja na dahalia.