SUA Yafanya Mapitio ya Mitaala ya Usimamizi wa Rasilimali Nyuki Kupitia Ushiriki wa Wadau wa Elimu

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kampasi ya Mizengo Pinda, kipo katika hatua ya kuboresha mitaala ya Shahada ya Sayansi ya Usimamizi wa Rasilimali Nyuki na Stashahada ya Sayansi ya Usimamizi wa Rasilimali Nyuki. Ili kuhakikisha mafanikio ya mchakato huu, chuo kilifanikiwa kuandaa warsha muhimu na wadau wa elimu Mkoani Tabora tarehe 22.12.2023. Lengo kuu la warsha hiyo ilikuwa ni kupitia upya mitaala ya Elimu ya Shahada ya Sayansi ya Usimamizi wa Rasilimali Nyuki na Stashahada ya Sayansi ya Usimamizi wa Rasilimali Nyuki.

Warsha hiyo ilihusisha washiriki kutoka makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wanachuo, wahadhiri, watafiti, wafugaji wa nyuki, na wadau wengine wa sekta ya nyuki. Kupitia majadiliano na mijadala mbalimbali. Katika warsha hiyo, washiriki walijadili kwa kina kuhusu mabadiliko yanayopendekezwa kwenye mitaala na kutoa maoni yao yanayolenga kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa na chuo.

Washiriki walitumia utaalamu wao na uzoefu wa kazi katika sekta ya nyuki kuchangia katika kuboresha maudhui ya mitaala, kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa inakidhi mahitaji ya soko na inazingatia mabadiliko na mwenendo wa hivi karibuni katika sekta hiyo muhimu.

Matokeo ya warsha hii yatachukuliwa kwa umakini na chuo, na yatafanyika marekebisho yanayostahili kwenye mitaala, kuzingatia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau wa elimu. Hii ni sehemu ya jitihada za chuo katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu inayokidhi viwango vya hali ya juu na inayolingana na matakwa ya soko la ajira.

Aliyesimama kutoka kushoto ni Mr Jackson Kizeze kutoka TAWIRI Tabora akichangia katika warsha ya wadau wa Elimu iliyofanyika Mkoani Tabora

Katika warsha hiyo, wadau wa elimu walipata nafasi muhimu ya kuchambua kwa kina mitaala inayohusu Usimamizi wa Rasilimali Nyuki. Walitumia fursa hiyo kutoa maoni yao yanayohusu ubora, uhalisia, ufanisi, na changamoto za mitaala hiyo. Miongoni mwa maoni muhimu yaliyotolewa ilikuwa haja ya kuhakikisha kuwa mitaala ya Usimamizi wa Rasilimali Nyuki inakidhi mahitaji na mazingira ya wafugaji wa nyuki Nchini Tanzania. Hivyo, kuna ulazima wa mitaala hiyo kujumuisha masuala ya kisera, kisheria, kiuchumi, kijamii, na kimazingira yanayohusiana na ufugaji wa nyuki.

Washiriki walisisitiza umuhimu wa mitaala kutoa msisitizo wa kuimarisha ujuzi na uwezo wa wanachuo katika kufanya utafiti, kuonyesha ubunifu, na kukuza ujasiriamali katika sekta ya nyuki. Aidha, kuna umuhimu wa kuongeza uwiano wa masomo ya nadharia na vitendo, na kuwapa wanafunzi fursa za kujifunza kupitia mafunzo ya vitendo, ziara za kiufundi, na miradi ya kuhitimu.

Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa mitaala inaundwa kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya nyuki, kama vile taasisi za utafiti, mashirika ya maendeleo, asasi za kiraia, na sekta binafsi. Hii inaweza kufanikiwa kwa kujumuisha masomo yanayohusu ushirikiano, ushauri, uhamasishaji, na uongozi katika mazingira ya ufugaji nyuki. Hatua hizi zinalenga kutoa elimu bora inayokidhi mahitaji ya soko na kuchangia maendeleo endelevu katika sekta ya nyuki.

Katika picha aliyesimama ndugu  James V. Lyamuya kutokea TAFORI Mkoa wa Tabora akichangia katika warsha ya wadau wa Elimu iliyofanyika Mkoani Tabora

 

Related Posts

Learning Through Practice: SUA Students Visit Weather Station

At the Sokoine University of Agriculture (SUA) Mizengo Pinda Campus, the focus on experiential learning continues to set students apart...

SUA Kampasi ya Mizengo Pinda Yasheherekea Miaka 63 ya Uhuru Katika Mdahalo Ulioandaliwa na Halmashauri ya Mpimbwe

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda, Ndg. Joseph Oswald Ruboha, akitoa mada ya...

Jinsi Mradi wa Elimu ya Juu kwa  Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), Unavyochochea Maendeleo ya SUA Kampasi ya Mizengo Pinda

Katika picha mwenye tai nyekundu: Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda, akitoa maelezo...