Utafiti: Ushirikina Wazuia Wanawake Kufanya Uvuvi

IMANI za kishirikina zinaelezwa kuwazuia wanawake kushiriki katika shughuli za uvuvi wa samaki kwenye maziwa na bahari, hivyo shughuli hizo kulazimika kufanywa na wanaume pekee.

Mtafiti kutoka chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi, Profesa Anna Sikira, alisema hayo wakati akitoa taarifa ya matokeo ya awali ya utafiti wake kuhusu changamoto za kijinsia na ushiriki wa wanawake katika mnyororo wa mazao yatokanayo na ziwa Tanganyika. Utafiti huo uko chini ya mradi wa Fish4ACP ambao unatekelezwa na shirika la Kimataifa la Kilimo na chakula (FAO).

Majadala kati ya mtafiti na wanakijiji
Mtafiti akifanya majadiliano na wanakijiji

Prof. Anna Sikira, ambaye ni Kaimu Rasi wa Ndaki ya Kampasi ya Mizengo Pinda (Taaluma), alieleza kwamba mojawapo ya changamoto ni wanawake kuzuiliwa kushiriki shughuli mbalimbali zinazohusiana na uvuvi wa Samaki. Sababu moja inayosababisha jambo hilo ni imani za kishirikina. Mathalani, inaaminika kuwa mwanamke akienda kuvua na hasa akiwa katika siku zake za hedhi ni mkosi na hivyo samaki hawawezi kupatikana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha wavuvi mwambao wa Ziwa Tanganyika, Francis Kabula amekiri kuwepo kwa vitendo vya kishirikina kwa baadhi ya wavuvi na kubainisha kwamba hali hiyo inatokana na kushindwa kujikita kwenye imani za kidini.

Mwenyekiti huyo amekiri kuwa kumekuwa na ubaguzi na unyanyapaa kwa wanawake kuingia ziwani kuvua kutokana na hali ya kuwa kwenye siku zao za hedhi kuonekana kama mkosi wanapojishughulisha na shughuli za uvuvi. Na kwamba ikiwa wanawake watagusa nyavu au kuingia kwenye mtumbwi basi samaki hawatapatikana.

Mratibu wa FAO ziwa Tanganyika

Akizungumzia kufanyika kwa utafiti huo Mratibu wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO), Hashim Muumin alisema kuwa utafiti huo unalenga kubaini changamoto, fursa na kutengeneza mpango ambao utawezesha kuondoa changamoto hizo na kuinua ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za uvuvi.

Muumini alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za uvuvi ni mdogo sana na katika maeneo mengine ya mnyororo mzima wa samaki wanawake hawapo kabisa. Hivyo, mradi huo unalenga kuongeza kipato kwa watu wote wanaojishughulisha na uvuvi na mazao ya uvuvi.

Hata hivyo, utafiti uliofanywa ulibaini kuwa ziko sababu nyingi za kisayansi zinazofanya samaki wasipatikane ambazo hazihusiani na ushiriki wa wanawake katika shughuli za uvuvi. Sababu hizo ni Pamoja na uharibifu wa mazingira na uvuvi haramu. Kwa mfano, katika miaka ya karibuni kina cha ziwa kiliongezeka na hivyo kuharibu mazalia ya Samaki. Aidha, uvuvi haramu umefanya wavuvi wavue hadi mazalia ya Samaki na hivyo kupunguza upatikanaji wake.

Pia, utafiti huo ulionyesha kwamba sehemu kubwa ya wanawake wanabaki kuwa wachakataji tu. Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 78 ya wachakataji wa mazao ya uvuvi kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika ni wanawake. Hata hivyo, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi katika shughuli hiyo.

Wanaume wakifanya uvuvi na wanawake wakiuza samaki waliochakata
Wanaume hasa ndio hufanya shughuli za uvuvi huku wanawake wakibaki kuwa wachakataji tu

Changamoto moja ni kutokua na soko la nje. Hii inatokana na ukweli kwamba wanawake wanaochakata samaki wana mitaji midogo na hivyo wanashindwa kufikia masoko na kupata kipato cha kutosha kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kaya zao. Isitoshe, uchakataji huo unafanyika kwa kutumia vifaa duni kama vile kuni ili kukausha samaki kwa moshi. Uchakataji huu hauwapatii viwango bora vya mazao yatokanayo na uvuvi, ni hatarishi kwa afya zao na si rafiki kwa mazingira.

Uchakataji duni wa samaki
Ukaushaji wa samaki kwa kutumia kuni haukidhi viwango, ni hatarishi kwa afya na mazingira

Zaidi ya hayo, vijiji vingi vya wavuvi havina miundombinu ya barabara, na ukweli ni kwamba mazao yatokanayo na samaki huharibika haraka na hivyo wakati mwingine kulazimika kumwaga/kutupa. Wadau walijadili swala hili na kuishauri FAO kuwapatia vifaa vya kisasa ili kupunguza hasara kwa wadau hawa.

Watafiti wakisafiri kwa boti
Watafiti wakitumia boti ili kufikia vijiji vilivyo kando ya ziwa Tanganyika

Mwishowe wadau walikubaliana kwamba iwapo wavuvi watatumia teknolojia ya kisasa ili kuongeza upatikanaji wa Samaki, habari ya ushirikina itakosa maana kabisa kwa kuwa wavuvi watapata Samaki wa kutosha kukidhi mahitaji yao.

Related Posts

Former Prime Minister Mizengo Pinda Visits Mizengo Pinda Campus to Observe Development Activities

The Mizengo Pinda Campus of Sokoine University of Agriculture (SUA) in Katavi recently hosted an esteemed visitor, Hon. Mizengo Pinda,...

Learning Through Practice: SUA Students Visit Weather Station

At the Sokoine University of Agriculture (SUA) Mizengo Pinda Campus, the focus on experiential learning continues to set students apart...

SUA Kampasi ya Mizengo Pinda Yasheherekea Miaka 63 ya Uhuru Katika Mdahalo Ulioandaliwa na Halmashauri ya Mpimbwe

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda, Ndg. Joseph Oswald Ruboha, akitoa mada ya...